Changamoto Za Kutafsiri Constitution of Kenya 2010 – Mkinzano Wa Kiisimu Na Usawidi Wa Kisheria: Kifani Cha Sura Ya 3 Na Sura Ya 4
Abstract
Utafiti huu unahusu changamoto za kutafsiri Constitution of Kenya 2010 kwa kuangazia ulinganifu wa maana unaoibushwa na mikinzano ya kiisimu na kwa njia hiyo kukinza uibukaji wa maana ya kisheria kwa mujibu wa uzingatiaji wa kanuni na matarajio ya usawidi wa kisheria. Kuwepo kwa makosa, hasa utohakika wa maana, unaotokana na tafsiri inayoibushwa katika Constitution of Kenya 2010 kunakisiwa kulichangiwa na matumizi ya mitazamo na mikakati banifu iliyoegemezwa tu katika usahihi wa kiisimu na kupembeza ulazima wa kusawazisha usahihi wa kiisimu na ufaafu wa usawidi wa kisheria. Uhalisi huu unaojitokeza katika kazi lengwa yaani, tafsiri ya Constitution of Kenya 2010 ulichochea haja ya kuhitajika kwa utafiti ili kubaini changamoto zinazojitokeza katika kuitafsiri Katiba kama matini ya kisheria. Malengo ya utafiti yalikuwa kuonyesha utohakika na ukinzani wa maana unaojitokeza katika kutafsiri dhana, kauli na istilahi za kisheria kutoka Kiingereza hadi Kiswahili, hasa kwa kuangazia tafsiri ya Sura ya 3 na Sura ya 4 ya Constitution of Kenya 2010. Utafiti huu unatathmini sababu zilizochangia kutokea kwa utohakika na ukinzani wa maana katika tafsiri ya Sura ya 3 na Sura ya 4 ya Constitution of Kenya 2010, kuchanganua athari zake kwa wapokezi wa Katiba hii katika lugha ya Kiswahili na kupendekeza mbinu mwafaka za kutatua ukinzani huu. Data iliyotumika kufanya uchanganuzi wa masuala ya tafsiri ilitolewa kutoka kwenye Sura ya 3 na Sura ya 4 ya Constitution of Kenya 2010. Uchanganuzi uliofanywa kubaini utohakika na ukinzani wa ulinganifu wa maana uliegemezwa katika misingi ya nadharia ya Skopos, hasa kwa kuzingatia kipengele cha nadharia hii kinachosisitiza uamili wa matokeo ya tafsiri yoyote ile, zikijumuishwa tafsiri za matini za kisheria. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa kulikuwa na ukinzani wa kimaana uliojitokeza katika sura hizi. Pia utafiti huu ulibaini kwamba uwepo na utohakika wa maana na ukinzani wa maana ni matokeo ya matumizi ya uelewa potofu na mbinu ambazo hazikusawazisha madai ya kiisimu na madai ya usawidi wa kisheria.
Publisher
University of Nairobi
Rights
Attribution-NonCommercial-NoDerivs 3.0 United StatesUsage Rights
http://creativecommons.org/licenses/by-nc-nd/3.0/us/Collections
The following license files are associated with this item: