Fani Katika Maulidi Ya Nuni
Abstract
Somo letu la utafiti limekuwa fani katika Maulidi ya Nuni. Malengo yetu ya utafiti yalikuwa ni kuchunguza nafasi ya wahusika na uhusika katika Maulidi ya Nuni na vilevile kuchanganua matumizi ya lugha, tamathali za usemi, muundo na mandhari katika Maulidi ya Nuni. Tumetumia nadharia ya mtindo ambayo ni mwafaka katika utafiti wetu. Tumeweza kuchunguza nafasi ya wahusika na uhusika kwa kutumia mbinu ya usimulizi ambapo mhusika amesawiriwa kupitia usimulizi, wasifu wake, msukumo wa matendo yake, tabia na amali zake. Katika matumizi ya lugha tumechunguza lahaja ya Kiamu, Kingozi na lugha ya Kiarabu. Katika tamathali za usemi tumechunguza ukiushi ambapo kifungu fulani hutumiwa kwa maana ambayo ni tofauti na maana ya kimsingi. Kutokana na hali hii, tumechunguza matumizi ya takriri, tashbihi, istiari, tashihisi pamoja na chuku. Vilevile tumechunguza matumizi ya taswira au jazanda na tumeona kuna picha zinazojitokeza ambazo zimefafanua tukio au hali fulani ya mhusika. Katika muundo, tumerejelea umbo na mpatano, mshikamano na uhusiano wa visehemu tofauti vya kazi hii ambavyo huleta sifa zinazotenganisha na kutambulisha mtunzi. Vilevile tumechunguza uhuru wa kishairi kwa kushughulikia inkisari, mazida pamoja na tabdila. Wahusika wameweza kuwekwa wazi kwa njia ambayo inadhihirika sana na mandhari. Utafiti huu ni wa kifasihi na umejikita katika fasihi andishi, kwa hivyo tumefanya kazi nyingi maktabani kwa kusoma kwa kina Maulidi ya Nuni yenye beti 130. Pia tumesoma kazi mbalimbali zilizogusia vipengele vya fani tulivyovishughulikia kama vile tasnifu mbalimbali, makamusi, vitabu vya ushairi na miswada mbalimbali. Tumeweza kusoma vitabu mbalimbali vya dini vikiwemo Qur‟an Tukufu na vitabu vyengine vya dini vilivyotusaidia. Tumewajumuisha walimu wa madrasa wakiwemo mashehe ambao walitupa mwongozo na mawazo. Tumepitia mtandaoni ili kupata yaliyofanywa kuhusu mada yetu ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwa kuna wahusika aina mbalimbali waliojitokeza katika kazi hii na wamejitokeza kama wahusika wa kawaida, wasiokuwa wa kawaida, wahusika wakuu, wahusika wasaidizi na pia wahusika wadogo kulingana na sifa zao. Katika matumizi ya lugha, tumebaini matumizi ya lahaja ya Kiamu, Kingozi na pia maneno ya Kiarabu. Kwa upande wa tamathali za usemi tumebaini matumizi ya takriri, tashbihi au tashbiha, istiari, uhuishaji au tashihisi, pamoja na chuku. Pia tumebaini matumizi ya taswira au jazanda. Katika muundo tumebaini umbo na mtindo wa utungo huu na pia uhuru wa kishairi kutokana na matumizi ya inkisari, mazida na tabdila. Katika mandhari au mahali tumebaini mandhari ya kijiografia, mandhari yasiyo halisi, mandhari ya kiishara, mandhari ya Uarabuni na pia mandhari ya kimapatano.Utafiti wetu umejikita kwenye fani katika Maulidi ya Nuni. Tunapendekeza kuwa watafiti wa baadaye washughulikie kipengele cha maudhui ambacho hatukukigusa. Vilevile tumetumia nadharia ya mtindo katika kushughulikia kazi hii. Tunapendekeza watafiti wa baadaye watumie nadharia tofauti na yetu katika kuchunguza utungo huu au tungo zengine.
Publisher
University of Nairobi
Subject
SwahiliRights
Attribution-NonCommercial-NoDerivs 3.0 United StatesUsage Rights
http://creativecommons.org/licenses/by-nc-nd/3.0/us/Collections
The following license files are associated with this item: