Show simple item record

dc.contributor.authorIkuathu, Silas T.
dc.date.accessioned2024-02-01T10:24:14Z
dc.date.available2024-02-01T10:24:14Z
dc.date.issued2022
dc.identifier.urihttp://erepository.uonbi.ac.ke/handle/11295/164267
dc.description.abstractTasnifu inahusu uchunguzi wa muundo na usimulizi katika riwaya ya kiupelelezi ya Kiswahili. Ili kufanikisha uchunguzi huu, malengo matatu yalizingatiwa. Malengo hayo yalikuwa; kuchunguza usimulizi katika riwaya ya kiupelelezi ya Kiswahili, kutathmini usawiri wa wahusika katika riwaya teule za kiupelelezi za Kiswahili na mwisho, kuchunguza mbinu za ujenzi wa msuko katika riwaya teule za kiupelelezi za Kiswahili. Kuhusu lengo la kwanza, utafiti huu ulichunguza vipengele vya usimulizi vya mtazamo na sauti za kisimulizi. Kuhusu lengo la pili, utafiti huu ulijikita katika utathmini wa jinsi wahusika wa riwaya ya kiupelelezi wanavyosawiriwa kwa njia maalum inayowapambanua na wahusika wapatikanao katika tanzu nyinginezo za riwaya. Ili kutekeleza lengo la tatu, mbinu za kimtindo zitumikazo kuukuza msuko wa riwaya teule zilichunguzwa. Data ya kimsingi iliyotumika ilipatikana kutoka kwa riwaya za kiupelelezi za waandishi mbalimbali. Hizi ni riwaya tatu za Mohammed Said Abdulla za Mzimu wa Watu wa Kale (1960), Kisima cha Giningi (1968) na Duniani Kuna Watu (1974), riwaya mbili za Ben Mtobwa za Tutarudi na Roho Zetu (1984) na Salamu Kutoka Kuzimu (1987), riwaya mbili za Elvis Musiba za Njama (1984) na Uchu (2000), riwaya ya Godfery Levi ya Mpelelezi Hodari na Genge la Wezi (1975) na riwaya ya Simu ya Kifo (1960) ya Faraj Katalambulla na mwisho, riwaya ya John Simbamwene ya Kwa Sababu ya Pesa (1971). Ili kuafikia malengo ya kazi hii, tulitumia nadharia tatu ambazo ni nadharia ya utanzu, nadharia ya naratolojia na nadharia ya umitindo. Nadharia ya utanzu ilituwezesha kuhakiki sifa bainifu za utanzu wa riwaya za kiupelelezi. Nadharia ya naratolojia nayo ilitumika katika kuchanganua vipengele vya kisimulizi vya mtazamo pamoja na nafsi za usimulizi katika riwaya teule. Ili kushughulikia mbinu za kimtindo zinazofanikisha ujenzi wa msuko katika riwaya za kiupelelezi za Kiswahili, nadharia ya umitindo ilitumika. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa riwaya nyingi za kiupelelezi zimetumia mtazamo nje katika usimulizi wa matukio. Usimulizi wa aina hii unampa msimulizi uhuru wa kusimulia mengi na kwa njia yenye utendeti. Imegunduliwa kuwa suala la mtazamo linajitokeza katika sawia nne ambazo ni sawia ya kiitikadi, sawia ya kimwanda-wakati, sawia ya kisaikolojia na sawia ya kiisimu. Imebainika kuwa wahusika wakuu katika riwaya za kiupelelezi wanaweza kuwekwa katika makundi matatu ambayo ni; waahusika wahalifu, wahusika wahasiriwa na wahusika wapelelezi.Makundi haya yanaweza pia kujitokeza kwa mtindo wa uwili; yaani, mpelelezi na msaidizi wake, mpelelezi na mhalifu na mhalifu na mpelelezi. Kuhusu msuko, utafiti huu umebainisha kuwa riwaya ya kiupelelezi huwa na usambamba wa hadithi mbili zikiwa ni hadithi ya uhalifu na ile ya uchunguzi. Ili kufikia muwala wa msuko huu, mbinu kadhaa hutumika. Mbinu hizo ni taharuki, mbinu rejeshi, usambamba, sadfa, hotuba miongoni mwa mbinu nyinginezo. Muundo wa kimsuko wa riwaya hizi unasalia kuwa sahili, usiokuwa na hadithi tegemezi nyingi wala mbinu rejeshi changamano. Uwepo wa msuko sahili ni sifa kuu inayorahisisha usomekaji na kuzifanya riwaya za kiupelelezi kuainishika kama fasihi pendwa.Utafiti huu unapendekeza utafiti zaidi ufanywe kuhusu riwaya ya kiupelelezi ya Kiswahili hususan kuhusu tanzu nyinginezo za kifasihi kama vile drama, hadithi fupi na mashairi kwa lengo la kubaini ikiwa kuna tamthilia au hadithi fupi za kiupelelezi katika fasihi andishi ya Kiswahili..en_US
dc.language.isootheren_US
dc.publisherUniversity of Nairobien_US
dc.rightsAttribution-NonCommercial-NoDerivs 3.0 United States*
dc.rights.urihttp://creativecommons.org/licenses/by-nc-nd/3.0/us/*
dc.subjectMuundo, Usimulizi, Riwaya Ya Kiupelelezien_US
dc.titleMuundo Na Usimulizi Katika Riwaya Ya Kiupelelezi Ya Kiswahilien_US
dc.typeThesisen_US


Files in this item

Thumbnail
Thumbnail

This item appears in the following Collection(s)

Show simple item record

Attribution-NonCommercial-NoDerivs 3.0 United States
Except where otherwise noted, this item's license is described as Attribution-NonCommercial-NoDerivs 3.0 United States