dc.description.abstract | Katika utafiti huu tumeshughulikia ukandamizaji wa jinsia ya kiume katika riwaya teule za
Kiswahili: Njozi Yapata Mtenzi ya Mwenda Mbatiah (2018) na Nguu za Jadi ya Clara
Momanyi (2019). Malengo ya utafiti huu ni: Kuchunguza makundi ya watu wanaokandamiza
jinsia ya kiume, kubainisha athari za ukandamizaji wa jinsia ya kiume na kuchunguza
mikakati ambayo wanaume wanatumia katika kupigania ukombozi wao katika riwaya teule
za Kiswahili: Njozi Yapata Mtenzi (2018) na Nguu za Jadi (2019). Zaidi ya hayo, nadharia
iliyotumiwa katika utafiti huu ni Nadharia ya Uwezo-Mkuu wa Kiume. Nadharia hii
iliasisiwa na Connel, R. (1987) na kuendelezwa na Bly, R. (1990) na baadaye Izugbara
(2005). Nadharia hii humchora mwanaume akiwa mbabe kwa misingi ya rangi nyeupe ya
ngozi na ya kibayolojia, humuona mwanaume kama mtekelezaji wa majukumu yote ya
familia na jamii yake kulingana na mila, itikadi na matarajio ya jamii na pia, hueleza kuwa
katika jamii kuna mwanaume mpya ambaye sio mbabe nyakati zote na hana tabia za mfumo dume ambazo huashiria kuwepo kwa taasubi ya kiume. Matokeo ya utafiti huu ni pamoja na:
Jinsia ya kiume imeonyeshwa kwa pande mbili. Kwanza, kuna wanaume wabinafsi ambao
wanatumia ubabe wao kuwakandamiza wanaume ambao sio wababe. Pili, kuna wanaume
wapya walioondokana na mfumo-dume, wanawajali wengine na wanandeleza ustawi wao,
wanaume wengine na jamii yao. Utafiti huu utakuwa muhimu katika taaluma ya elimu jamii
kuwahamasisha kuhusu masuala ya mahusiano mema ya kiuana na usawa wa kijinsia. Aidha,
utafiti huu utakuwa muhimu katika kuendeleza taaluma ya Kiswahili hususan fasihi ya
Kiswahili hasa katika uandishi wa riwaya ambao huzidi kukua na kubadilika na waandishi
chipukizi wa riwaya watanufaika zaidi. Kadhalika, utafiti huu utatumika kuhamasisha jamii
kuwa sio wanawake ambao hukandamizwa tu pia wanaume hukandamizwa na kuna haja ya
kuangalia upya suala la ukandamizaji wa jinsia zote. Pia, utafiti wetu utatumika na watafiti
wa baadaye katika kuendeleza tafiti zao. | en_US |