dc.description.abstract | Tumeangazia taswira ya mwanamke katika tamthilia za Nguzo Mama na Mama Ee. Jamii
mbalimbali zina mtazamo anuai kuhusu taswira ya mwanamke. Waandishi wa tamthilia hizi
walitoka maeneo tofauti na waliandika katika vipindi tofauti, lakini kazi zao zinashabihiana sana.
Tulichagua mada yetu ili kuchambua na kuchanganua tamthilia za Nguzo Mama na Mama Ee
kwa sababu ya fani na maudhui yanayoashiria jinsi hali halisi ilivyo katika jamii zetu. Malengo
ambayo tumeyaangazia ni jinsi changamoto mbalimbali zinamkabili mwanamke na kumzuia
kupata haki, jinsi asasi za kijamii zinavyochangia mwanamke kutopata mafanikio katika harakati
zake za kutaka kujikomboa na kuonyesha jinsi baadhi ya waandishi wamemsawiri mwanamke
kwa njia mbalimbali kama vile shujaa, mwongo mwoga na kadhalika.
Tuliweza kujikita kwenye vitabu hivi viwili tu, Nguzo Mama na Mama Ee isipokuwa pale
tulipohitaji kutoa idhibati au mifano zaidi. Dira iliyotuongoza kuangazia mada yetu ni nadharia
ya Sosholojia ya Fasihi iliyoasisiwa na Georg Lucaks mwanaitifaki wa Karl Marx. Nadharia hii
ya Sosholojia ya Fasihi ni kitengo maalum cha uchunguzi ambacho humulika mahusiano baina
sya kazi ya sanaa hasa fasihi, umma na muundo wa kijamii.
Baadhi ya changamoto tulizofanikiwa kugundua katika uchambuzi wetu ni matatizo ya
unyumba, ubaguzi wa kijana wa jinsia ya kike, mila na desturi katika ndoa, dini katika
mahusiano ya kinyumba, mahakama za kiserikali na zile za kijijini, ukosefu wa umoja na
ushirikiano, utabaka,na majukumu mengi miongoni mwa zingine. Asasi za kijamii hasa ndoa na
tamaduni zilionekana kuchukua nafasi ya vizingiti vikuu na kumfanya mwanamke kuwa na
taswira mbalimbali. Kwa mfano mwanamke amechorwa kama mwoga, mwenye chuki na wivu,
mwenye tamaa, mwenye mashaka na mdhaifu miongoni mwa nyingine.
Tulitamatisha kazi yetu kwa kutoa mapendekezo mawili. Pendekezo la kwanza linahusiana na
dini. Swala la dini kuchangia katika unyanyaswaji wa mwanamke yafaa lichunguzwe kwa
undani zaidi. Pendekezo la pili linahusiana na suluhu la kudumu kuhusu changamoto
zinazomkumba mwanamke katika jamii na kumnyima uhuru kamili. | en |