dc.description.abstract | Lengo la utafiti huu lilikuwa ni kutathmini na kuchanganua makosa ya kimofosintasia
katika lugha ya kimaongezi kwa wanafunzi na walimu katika kaunti ndogo ya Kangema.
Walimu na wanafunzi tuliojihusisha nao walikuwa ni wakazi wa eneo hilo na lugha yao
ya kwanza ilikuwa ni Kikuyu. Tulitumia mtazamo wa Uchanganuzi Makosa. Nadharia
ya uchanganuzi Makosa iliasisiwa na corder na wenzake mnamo mwaka wa 1960. Kwa
mujibu wa nadharia hii makosa husababishwa na visababishi vingi mbali na athari ya
lugha ya kwanza. Nadharia hii vilevile inachangia katika kubaini mikakati ambayo
hutumiwa na wanafunzi katika harakati za ujifunzaji wa lugha ya pili na aidha kutambua
visababishi vya makosa na hata chanzo cha makosa mengi katika kazi za wanafunzi. Kwa
kuongozwa na nadharia hii basi, katika utafiti wetu, tuliyasikiliza makosa na kuyaandika,
kisha tuliyapanga kulingana na aina na hatimaye kuelezea kilichosababisha makosa hayo.
Kabla ya kuingia nyanjani na kufanya utafiti wetu tulikisia kwamba makosa mengi ya
kimofosintaksia yanayofanyika ni makosa ya kimatamshi. Tulikuwa pia tumetabiri kuwa,
makosa mengi ya kimofosintaksia hutokana na mazingira na athari za lugha ya kwanza za
wazungumzaji wa Kiswahili katika kaunti ndogo ya Kangema. Vile vile tulikisia kwamba
ukiushi wa kimofosintaksia katika matumizi ya lugha hujitokeza pale walimu
wanapowahutubia wanafunzi katika vikao rasmi na kwamba kuna uwezekano wa
kuyarekebisha makosa hayo. Tulichagua vikundi viwili vya watafitiwa ambao ni walimu
na wanafunzi. Tulichukua sampuli rahisi bila kufuata utaratibu wowote. Baada ya
kuyakusanya makosa kutoka kwa watafitiwa wetu, kuyaweka katika kategoria kulingana
na aina, tuliweza kudhibitisha makisio ya nadharia tete zetu. Tulifanyia utafiti wetu
katika shule za upili na za msingi katika kaunti ndogo ya Kangema. Tulishughulikia
mokosa ya kimofosintaksia pekee ingawa katika shughuli za kufanya hivyo tulijadili
makosa ya kimofolojia. Hii ni kwa sababu makosa ya kimofosintaksia yanaweza
kusababishwa na makosa ya kimofolojia. Tuliushughulikia ukiushi wa kimaongezi.
Hatukuchunguza ukiushi wa kimaandishi. Wahusika wetu wa utafiti walikuwa ni wale
wanaozungumza lugha ya Kikuyu kama lugha yao ya kwanza.Tulikuja kugudua kuwa
mengi ya makosa hayo yalisababishwa na athari za lugha ya kwanza ambayo ni Kikuyu.
Makosa hayo yalionekana yakiwa mengi sana katika viwango vya chini vya elimu na
kupungua kadri mwanafunzi alivyoendelea na masomo ya kiwango cha juu. Umilisi
ulionekana kuongezeka kadri kiwango cha e1imu kilivyoongezeka. Ilikuwa dhahiri kuwa
walimu waliongea kwa ufasaha zaidi kuliko wanafunzi ingawa hata wao walifanya
makosa hapa na pale. | en_US |