dc.description.abstract | Utafiti huu ulinuia kuchunguza athari za ulumbilugha kwa Kiswahili. Tasnifu hii
imegawanywa kwa sura tano. Katika sura ya kwanza tulishughulikia utangulizi wa kazi
hii kwa ujumla kwa kuangazia tatizo la utafiti, maswali na malengo ya utafiti huu, sababu
za kuchagua mada, yaliyoandikwa kuhusiana na mada yetu na vile vile mbinu za utafiti.
Katika sura ya pili, tulishughulikia dhana za ulumbilugha na kuchanganya ndimi na
hatimaye tuliangazia mielekeo ya wanafunzi kuhusu Kiingereza, Kiswahili na Sheng‟.
Tulijikita kwa athari hasi na chanya za Sheng‟ na Kiingereza kwa Kiswahili kwa
kuangazia insha za wanafunzi wa shule za msingi za CGHU na Moi Avenue. Kutokana
na data ya utafiti huu, tuligundua kuwa athari hasi ni nyingi zaidi ya athari chanya na hili
ni jambo linalowafanya wanafunzi wa shule za msingi za CGHU na Moi Avenue kupata
alama za chini katika uandishi wa insha za Kiswahili. Tulishughulikia athari hasi na
chanya za sheng‟ na Kiingereza kimofolojia katika sura ya tatu na vile vile kisintaksia
katika sura ya nne. Athari hasi za Sheng‟ na kimofolojia ambazo tulishughulikia ni:
ukataji wa silabi za Kiswahili kwa namna isiyofaa, kuandika ukubwa na udogo wa
nomino za Kiswahili visivyo na pia kunyambua vitenzi vya Kiswahili visivyo. Athari
hasi za Kiingereza tulizobaini katika mofolojia ni uswahilishaji maneno ambayo yana
msamiati uliozoeleka katika Kiswahili, matumizi ya konsonanti za Kiingereza katika
uandishi wa insha, kutumia maneno ya Kiingereza na uambishaji wa maneno ya
Kiswahili visivyo. Athari chanya ya ulumbilugha kimofolojia iliyobainika katika data ya
utafiti huu ni ufahamu wa maana za maneno. Katika sintaksia, tulishughulikia athari hasi
na chanya za ulumbilugha katika uandishi wa insha za Kiswahili. Tuliangazia sentensi
katika insha za watafitiwa wetu na tuligundua kuwa athari hasi za Sheng‟ kisintaksia ni:
matumizi ya mbinu ya uhuishaji pasipofaa, uongezeaji wa viambishi visivyo, kuendeleza
misamiati ya Kiswahili visivyo na matumizi ya maneno ya Sheng‟. Tulibaini kuwa pia
umilisi wa Kiingereza uliwaathiri kwa njia hasi kwa kuwa wanafunzi wa shule za msingi
za CGHU na Moi Avenue wanaendeleza viambishi vya nafsi visivyo, matumizi mabaya
ya vivumishi vya aina mbalimbali kama vile vivumishi vya a-unganifu, vionyeshi,
vimilikishi, virejeshi na vile vya idadi. Athari hizi hasi zinaifanya sentensi kutokuwa
sahihi na hivyo basi wanafunzi wanaadhibiwa kwa kufanya makosa ya kisarufi.
Hatimaye, tulishughulikia athari chanya za ulumbilugha kisintaksia na tulibaini kuwa
uliwawezesha wanafunzi wa shule za msingi za CGHU na Moi Avenue wanatunga
sentensi ambazo zimekamilika kimaana, sahihi na kimantiki. Hatimaye tulishughulikia
mahitimisho ya utafiti huu na mapendekezo kwa watafiti wa baadaye. | en_US |