Sentensi Sharti Ya Kiswahili Sanifu Na Ekegusii
Abstract
Lengo la tasnifu hii ni kufanya uchunguzi linganishi wa sentensi sharti ya Kiswahili
Sanifu na Ekegusii kwa kutumia nadharia ya Upanuzi wa Sarufi Sawazishi. Tumeigawa
kazi hii katika sura tano. Katika sura ya kwanza, tumetoa maelezo ya kimsingi
yanayohusu somo la utafiti, madhumuni ya utafiti na upeo wa tasnifu. Masuala mengine
ambayo yameshughulikiwa ni pamoja na sababu za kulichagua somo, nadharia tete,
yaliyoandikwa kuhusu somo hili, msingi wa nadharia na mbinu za utafiti.
Sura ya pili inalenga kushughulikia sintaksia ya sentensi sharti ya Kiswahili Sanifu. Sura
imeanza kwa kutoa fasili ya sentensi sharti ya Kiswahili na ufafanuzi wa viambajengo
vyake. Viambajengo hivi ni pamoja na kishazi sharti, kishazi shurutiwa, vitambulishi
sharti na viunganishi viambatishi. Vipashio vinavyotumiwa kutolea masharti
vimetambuliwa na kufafanuliwa. Vipashio hivi ni pamoja na ‘kama, ikiwa, endapo,
iwapo, ki, nga, ngali, nge na ngeli’. Suala lingine lililoshughulikiwa katika sura hili ni
muundo wa sentensi sharti ya Kiswahili na ugeuzi unaojitokeza katika kuigeuza sentensi
sharti kutoka kiwango cha muundo msingi hadi kile cha muundo geuzi. Imebainishwa
kuwa sentensi sharti ya Kiswahili ikiwa katika kiwango cha muundo msingi huwa na
kishazi shurutiwa mwanzoni kikifuatwa na kishazi sharti. Vishazi hivi huunganishwa
kwa mujibu wa kitambulishi sharti kinachokitegemeza kishazi sharti kwa kishazi
shurutiwa. Sentensi hiyo inapogeuzwa hadi kiwango cha muundo geuzi, kanuni ya ugeuzi
hukitanguliza kishazi sharti kikifuatwa na kishazi shurutiwa. Wakati wa ugeuzi huo,
kiunganishi kiambatishi kisicho cha lazima hutokea na kukitegemeza kishazi sharti kwa
kishazi shurutiwa.
Sura ya tatu inashughulikia fasili ya sentensi sharti ya Ekegusii na ufafanuzi wa
viambajengo vyake. Viambajengo hivi ni pamoja na kishazi sharti, kishazi shurutiwa,
vitambulishi sharti na viunganishi viambatishi. Imebainika kuwa sentensi sharti ya
Ekegusii huundwa kwa kishazi sharti na kishazi shurutiwa. Vitambulishi sharti katika
lugha ya Ekegusii ni pamoja na ‘onye, -ise, -are, k- na ebe’. Kuna kiunganishi
kiambatishi kitumiwacho ambacho si cha lazima kinachotumiwa kukiunganisha kishazi
sharti na kishazi shurutiwa. Kiunganishi hiki ni ‘rirorio’ ambacho hudhihirika katika
kiwango cha muundo geuzi pekee. Mengine yaliyoshughulikiwa katika sura hii ni
muundo wa sentensi sharti ya Ekegusii na ugeuzi unaojitokeza katika kuigeuza sentensi
sharti kutoka kiwango cha muundo msingi hadi kile cha muundo geuzi. Uchunguzi
umepata kuwa sentensi sharti ya Ekegusii ikiwa katika kiwango cha muundo msingi
huwa na kishazi shurutiwa kikitangulia mwanzoni mwa sentensi kikifuatwa na kishazi
shurutiwa. Kishazi sharti hutegemezwa kwa kishazi shurutiwa kwa matumizi ya
kitambulishi sharti kinachotekeleza pia jukumu la kutambulisha sharti. Sentensi sharti
hugeuzwa kutoka kiwango cha muundo msingi hadi muundo geuzi kutokana na ugeuzi
unaokitanguliza kishazi sharti kikifuatwa na kishazi shurutiwa. Ugeuzi huo husababisha
kutokea kwa kiunganishi kiambatishi ‘rirorio’ kisicho cha lazima na kinachoviunganisha
vishazi husika kwa kukitegemeza kishazi sharti kwa kishazi shurutiwa.
Katika sura ya nne, ulinganishi wa vipengele mbali mbali vinavyohusiana na sintaksia ya
sentensi sharti ya Kiswahili sanifu na Ekegusii umefanywa. Kumeshughulikiwa
uainishaji wa sentensi sharti ya Kiswahili na Ekegusii, kufanana na kutofautiana kwa
kishazi sharti cha Kiswahili na cha Ekegusii, kufanana na kutofautiana kwa miundo ya
sentensi sharti ya Kiswahili na Ekegusii na ulinganishi wa michakato ya ugeuzi
inayogeuza sentensi sharti kutoka kiwango cha muundo msingi hadi kile cha muundo
geuzi.
Sura ya tano inatoa mahitimisho ya kijumla ya tasnifu hii. Inaanganzia masuala muhimu
yaliyoshughulikiwa na mahitimisho yao katika kila sura ya tasnifu hii na kisha kutoa
mapendekezo kulingana na maoni ya mtafiti
Citation
Tasnifu Hii Imetolewa Kwa Madhumuni Ya Kutosheleza Baadhi Ya Mahitaji Ya Shahada Ya Uzamili Wa Sanaa Katika Chuo Kikuu Cha NairobiPublisher
University of Nairobi Faculty of Arts