dc.description.abstract | Utafiti huu unahusu suala la uhamaji na uhamiaji kama linavyoendelezwa katika riwaya ya
kitawasifu ya Mbali na Nyumbani iliyoandikwa na Adam Shafi. Suala la uhamaji na uhamiaji
ndilo lililotawala riwaya nzima kutoka mwanzo hadi mwisho. Mwandishi wa riwaya hii
ameathiriwa na suala hili la uhamaji na uhamiaji kwani ameyapitia hayo yote. Hii ndiyo sababu
riwaya yenyewe inaitwa ya kitawasifu. Uhakiki wetu umeongozwa na nadharia ya uhalisia
ambayo hujikita katika utoaji wa picha halisi ya maisha ya binadamu. Nadharia hii ina vipengele
vingi lakini sisi tumetumia vipengele vitatu. Hivi ni: Kipengele cha kihistoria, kisiasa na
kitamaduni. Kazi hii imelenga kushughulikia tatizo la utafiti ambalo linahusu uhamaji na
uhamiaji. Matatizo yanayowakumba wanajamii katika sehemu mbalimbali za ulimwengu hasa
mataifa ya ulimwengu wa tatu ndiyo yaliyotusukuma kufanya utafiti huu. Matatizo haya yanazidi
kuangaziwa kila uchao kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Aidha, tumechambua maudhui
yanayoingiliana na suala la uhamaji na uhamiaji katika riwaya husika. Sababu yenyewe ni
kwamba, maudhui hayo yanachangia katika kuboresha au kufanya maisha ya wahusika kuwa
magumu wakiwa katika hali ya uhamaji na uhamiaji. Si hayo tu bali tumefafanua aina za uhamaji
na uhamiaji zinazopatikana katika riwaya yenyewe. Vilevile, tumeangalia sababu zinazochangia
hali hiyo na manufaa ya uhamaji na uhamiaji. Zaidi ya hayo, tumeeleza kwa kina matatizo
yanayowakumba wahusika katika riwaya hii na jinsi wanavyojaribu kuyatatua. Katika utafiti
huu, tumegundua kuwa matatizo yanayowakumba wahusika katika riwaya hii ni yaleyale
yanayowakumba watu wengine wakiwa katika hali ya uhamaji na uhamiaji popote pale. Baada
ya kupata hayo, tunapendekeza kwamba, serikali na mataifa yaliyokumbwa na tatizo hili yajaribu
kuweka mikakati ya kuchunguza kiini chake na kutafuta njia za kulitatua kabla halijaharibu
mishikamano ya wanajamii. | en_US |