dc.description.abstract | Utafiti wa lugha kuegemea mitazamo ya kikompyuta umetamalaki katika lugha zilizoendelea
kidijitali kama Kiingereza na nyinginezo ila dhana hii haijakita mizizi kabisa katika utafiti wa
lugha za Kiafrika kama Kiswahili. Utafiti huu umeangazia suala la matumizi ya teknolojia ya
lugha katika utafiti wa Kiswahili kwa kuchunguza na kutathmini mbinu mbali mbali
zilizotumika katika mradi wa SALAMA (Swahili Language Manager), ulioasisiwa na Arvi
Hurskainen profesa wa taaluma za lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Helsinki nchini
Finland kutoka 1985- 2015 ili kutambua ukweli wa hali ya utafiti wa Kiswahili katika jukwaa
la teknolojia ya lugha. Kwa kutumia mazingira ya SALAMA, ambayo yalishughulikia
Kiswahili na kuchunguza nyanja zake mbali kwa kutumia programu zilizojengwa kwenye
misingi ya kanuni za lugha na za kikompyuta, utafiti huu ulilenga kubainisha mbinu
mbalimbali zilizohusika katika utafiti wa kikompyuta wa lugha ya Kiswahili katika mradi
huu na kuzichunguza mbinu hizo zilizotumika kufanyia utafiti na kuchanganulia vipengele
tofauti tofauti vya lugha hii, na iwapo zinaweza kuwa zimechangia katika kukuza na
kuendeleza utafiti wa Kiswahili kama lugha ya Kiafrika inayoweza kutafitiwa kwa kutumia
Teknolojia ya Lugha au Uhandisi Lugha. Katika kufanya hivi, Utafiti umelenga kuonyesha
umuhimu, uamilifu na utumiwaji wa kongoo au kopasi katika Teknolojia ya Lugha na jinsi
kanzi hii inavyoweza kuboresha utafiti katika lugha ya Kiswahili kikompyuta. Nadharia ya
Msambao wa Ugunduzi (Diffusion of Innovation Theory) iliyoasisiwa na Everett Rogers
(2003) pamoja na Nadharia ya Isimu Kongoo au Mtazamo wa Kikongoo zimetumika katika
kujaribu kueleza jinsi teknolojia ya lugha ni mkabala ulio na manufaa zaidi kiutafiti kuliko
mbinu za kimapokeo. Kupitia kwa data kutoka kwa hojaji na mifano kutoka kwa ripoti mbali
mbali na kazi za kitaaluma zinazohusu SALAMA, utafiti umebaini kuwa teknolojia ya lugha
inachangia katika utafiti ya kiujarabati zaidi, ina uwezo wa kuichakata data kubwa zaidi
kikompyuta kuliko uwezo wa binadamu, inampa mtafiti mnepo na uhuru zaidi, inahifadhi
lugha kikompyuta na inaweza kushughulikia lugha ya Kiswahili kiutafiti katika maeneo yote
kutoka uundaji na utathmini wa kamusi, tafsiri-mashine, uchanganuzi wa kimofolojia,
kisintaksia,kisemantiki,ufundishaji lugha na miongoni mwa masuala mengine. | en_US |