Fani katika ushairi wa Hassan Mwalimu Mbega: uhakiki wa upisho wa umalenga na dafina ya umalenga
Abstract
Tasnifu hii imeshughulikia fani katika ushairi wa Hassan Mwalimu Mbega.
Tumehakiki diwani zake mbili ambazo ni Upisho wa umalenga (1975) na Dafina ya
Umalenga (1984) kwa kutumia nadharia ya urasimu.
Kuna sura tano katika tasnifu. Sura ya kwanza ni ya utangulizi ama
pendekezo la utafiti. Ni sura inayohusu somo la utafiti, madhumuni ya utafiti, upeo
na mipaka ya utafiti, sababu za kulichagua somo, haipothesia, yaliyoandikwa kuhusu
somo, msingi wa nadharia na njia za utafiti.
Sura ya pili ambayo ni ya misingi ya uhakiki inahusu uamili wa lugha ya
kishairi katika sanaa, sifa zake, na namna inavyoshirikiana au kutumiwa katika ploti.
Tumeangalia umuhimu wa kila mojawapo ya vipengele hivyo na mchango wao katika
fani kwa jumla. Baada ya kuangalia mengi ya kifani ambayo ni mwongozo wa sura
zinazofuatia, tumezitamzama na kuzihakiki tungo za mwalimu Mbega katika misingi
ya yaliyopitiwa katika sura za kwanza na pili. Maswala ya nadharia ya urasimu na
mwongozo wake vimezingatiwa katika kuhakiki tungo hizo.
Sura ya tatu inahusu uhakiki kifani wa upisho wa umalenga, huku sura ya nne
ikishughulikia maswala ya kifani katika diwani ya Dafina ya Umalenga.
Sura ya tano ni hitimisho ambapo kwa njia ya muhtasari imethibitisha
haipothesia pamoja na kushughulikia maswala mengine ya kifani. Tasnifu hii ina sura
tano zinazoshughulikia maswala ya kifani.
Kwa sababu ambazo hatukuweza kuziepuka, alama za kufungia maneno
zimetokea zikiangalia upande mmoja. Hii ni kwa sababu, ya aina ya kompiuta
iliyotumiwa ambayo haina alama za kufungia. Tunaomba radhi kwa makosa hayo .
Citation
Masters of education thesis,University of Nairobi (1997)Publisher
University of Nairobi Department of Arts