Athari za sheng katika dini ya Kikristo: Mtaa wa Umoja.
View/ Open
Date
2013-10Author
Odhiambo, George O
Type
ThesisLanguage
otherMetadata
Show full item recordAbstract
Tasnifu hii ililenga kutathmini athari za Sheng katika dini ya Kikristo. Kwa jumla tasnifu hii ina
sura tano. Katika kila sura, tumeshughulikia maswala na vipengele maalum ambavyo
vinaingiliana na kukamilishana.
Katika sura ya kwanza tumeshughulikia usuli wa tasnifu hii. Tumetangulia kwa kutoa maana na
chimbuko la lugha ya Sheng. Vile vile tumefafanua kwa upana tatizo la utafiti, swala la utafiti,
nadharia tete, sababu za kuchagua mada husika, msingi wa kinadharia, upeo na mipaka ya utafiti,
njia za utafiti pamoja na umuhimu wa utafiti huu katika nyanja ya elimu na utafiti.
Katika sura ya pili tumejadili mbinu mbalimbali za uundaji wa maneno ya Sheng. Mbinu hizi za
uundaji wa maneno tumezichanganua kwa kukita katika kiwango cha isimu cha mofologia.
Katika michakato yetu ya kuzichanganua mbinu hizi za uundaji wa maneno katika Sheng,
tumeweza kabaini kwamba mengi ya maneno ya Sheng huwa yamekopwa kutoka katika lugha
zingine hususan Kiingereza, Kiswahili na Kikuyu. Maneno haya yaliyokopwa aidha hutoholewa
ili yachukue sauti na muundo wa kimofologia wa leksimu za Sheng (kibantu). pamoja na ukopaji
na utohozi, maneno ya Sheng pia yameundwa kwa mbinu zingine za uundaji wa maneno, kama
vile uambatishaji, uambishaji, upolisemia, onomatopia, uhulutishaji, ubunifu, kaleki, ujenzi
ghairi, akronimu, ukatizaji, ubadilishaji silabi na unyumbuzi kapa. Maneno ya Sheng ambayo
kiasili hayatokani na ukopaji ni maneno buniwa pekee. Mifano ya maneno haya asilia ya Sheng
ni pamoja na:
Sheng Tafsiri
Ndai = Gari
Nganya = Daladala
Ukedi = Ukimwi
Uchiwa = Urembo
Mbus = Msichana
- 12 -
Dingo = Mwizi
Bonoko = Gushi
Deng’a = Chuma
Hii ndio mifano ya maneno ambayo kiasilia tuliweza kubaini kwamba ni leksimu za Sheng.
Katika sura ya tatu tumeweza kubaini kwamba Sheng huzitumia lekisu hizo ilizojiundia kwa
mbinu mbalimbali za kimofologia ili kujiundia vifahiwa . Baadaye wanajamii lugha hii ya Sheng
huvitumia vifahiwa hivyo katika kujitungia sentensi. Sentensi hizo huwa za viwango mbalimbali
vya kisintaksia na kisemantiki na ndizo ambazo hufanikisha mawasiliano miongoni mwa
wanajamii lugha hii ya Sheng. Mifano ya vifahiwa hivyo vya Sheng tumevijadili kwa kuvitolea
tafsiri ya Kiswahili sanifu. Sentensi ambazo huundwa kutokana na vifahiwa hivi huwa
hazieleweki bayana na watu wasioielewa Sheng au wasiolengwa. Mojawapo ya watu hawa ni
Wakristo wenye umri wa juu kama vile wazazi pamoja na vijana wasioilewa Sheng. Kundi hili la
watu wasioielewa Shenge huitwa “fala,” jina ambalo huwa na lengo la kuwadunisha na
kuwafedhehesha watu hawa. Kwa kiwango kikubwa, sentenzzi hizi za Sheng tumeweza
kuzichanganua kwa vigezo vya kisintaksia ila kwa juujuu tu. Hii ilitokana na sababu kwamba
tulilenga kukita katika semantiki wala sio katika sintaksia. Hata hivyo matawi haya mawili yote
huingiliana na kukamilishana kwa ujumla na misingi ya isimu.
Katika sura ya nne tumepata kufahamu kwamba wanajamii lugha ya Sheng huzitumia sentensi
ilizojiundia kutokana na vifahiwa mbalimbali kwa kujieleza hasa kupitia sanaa ya uimbaji.
Nyimbo ambazo tumeziangazia ni nyimbo za Kikristo wala sio za kidunia. Hii ilitokana na
sababu kwamba utafiti wetu ulikita katika kutathmini athari za Sheng katika dini ya Kikristo.
Hivyo tumepata kubaini kwamba Sheng ina athari zake katika asasi na taasisi mbalimbali za
kijamii na kidini. Mifano ya taasisi na asasi hizi ni pamoja na makanisa (ya awali na ya kisasa
nchini Kenya), na vyombo vya habari. Mifano ya makanisa ya awali tuliochanganua ni pamoja
na kanisa la Katoliki, kanisa la SDA, kanisa la Angilikana, kanisa la PCEA, kanisa la A.C.K na
kanisa la ‘Quackers. Mifano ya makanisa ya kisasa ambayo tumeangazia ni pamoja na “The
Holy Ghost Fire Ministry”, “Jesus is Alive Ministry”, na “God’s Favour Ministry”
- 13 -
Kati ya aina hizi mbili za makanisa, tumepata kubaini kwamba makanisa ya kisasa ndiyo
ambayo yamekubali matumizi ya Sheng kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha taratibu za
ibada. Athari za Sheng katika makanisa ya awali bado hazijaanza kuchipuza ingawaje dalili zipo.
Taasisi nyngine ya kijamii ambayo tuliweza kubaini kwamba athari za Sheng hujithirihisha
kwayo ni taasisi ya habari na mawasiliano. Mifano ya vyombo vya habari ambavyo
tumeviangazia ni redio, televisheni na vijisahani vya santuri.
Katika sura ya tano, tumeweza kujadili hitimisho la tasnifu hii. Vile vile tumeweza kujadili
mambo ibuka ambayo hatukuwa tumeyajumuisha katika malengo na haipothesia zetu. Mambo
haya ibuka ni pamoja na Sheng kutumiwa kwa kuyabuni makundi maovu ya watoto ambayo
yana lengo la kuwafundisha na kuwahimiza watoto wasiwatii wazazi wao na watu wazima.
Mfano wa kundi la aina hii ambalo tuliweza kulibaini ni kundi linalojulikana kama “Gaza”. Pia
katika sura hii ya tano tumengazia maswala ya kijumla hususan yanayohusu matokeo ya utafiti
wetu. Aidha tumependekeza baadhi ya maswala ambayo watafiti wa baadaye wataweza
kuyaangazia kwa kina katika tafiti za baadaye.
Citation
Shahada Ya Uzamili Katika Chuo Kikuu Cha Nairobi.Publisher
University of Nairobi Department Of Linguistics And Languages