Mtindo katika diwani ya mfuko mtupu na hadithi nyingine
Abstract
Tasnifu hii imeshughulikia mtindo katika Mfuko Mtupu na Hadithi Nyingine.
Katika sura ya kwanza, mambo muhimu yanayojadiliwa ni; Utangulizi, Tatizo la Utafiti,
Madhumuni ya Utafiti, Nadharia Tete, Sababu za Kuchagua Mada, Upeo na Mipaka ya tasnifu,
Msingi wa Nadharia ya Utafiti, Yaliyoandikwa kuhusu mada hii na mwisho ni njia tulizotumia
kukamilisha utafiti huu.
Katika sura ya pili, utafiti wetu umejikita katika kuchunguza matumizi ya msamiati katika Mfuko
Mtupu na Hadithi Nyingine. Tumeshughulikia jinsi mwandishi ameteua msamiati wake ili
kuwasilisha ujumbe anaodhamiria kufikisha kwa hadhira yake.
Sura ya tatu inahusu uchanganuzi wa mtindo kwa misingi ya kisintaksia katika Mfuko Mtupu na
Hadithi Nyingine. Tumechunguza ukiushi katika baadhi ya kategoria za maneno. Pia tumejadili
ukiushi katika sentensi ndefu, fupi na nafasi ya uakifishaji katika sintaksia ya diwani yenyewe.
Tumemalizia sura hii kwa kujadili ukiushi unaoibuka kwa kutozingatia muundo wa kiima
kiarifa.
Katika sura ya nne, tumechanganua ukiushi wa kisemantiki katika diwani ya kazi hii ya Said
Mohamed . Tumechunguza tamathali za usemi kama tashbihi, sitiari, kinaya, tashhisi, tanakuzi,
majazi, tasifida, maswali ya balagha na chuku. Pia tumechunguza mbinu nyingine za lugha kama
takriri, usambamba wa visawe, tanakali za sauti, kuchanganya ndimi, jazanda, methali, barua na
nyimbo.
Sura ya tano tumehitimisha kwa kurejelea yale tuliyojadili katika sura za awali hasa kwa
kuangaza madhumuni, nadharia tete na nadharia tuliyotumiwa kuhakiki kazi hii. Kadhalika
tumeonyesha mchango wetu kutokana na yale ambayo tumeshugulikia katika utafiti huu.
Hatimaye, tumetoa mapendekezo yetu kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili.
Publisher
University of Nairobi, Department of Kiswahili