Matatizo yanayodhihirika katika matini tafsiri za kimatibabu: utafiti kielelezo katika Hospitali ya Kisii level 5
Abstract
Utafiti wetu unahusu matatizo yanayodhihirika katika matini tafsiri za kimatibabu. Kwa kuwa
taaluma ya kimatibabu ni pana, tuliteua sehemu nne za kurejelea katika utafiti huu. Sehemu hizi
ni: magonjwa kwa jumla, dalili au ishara za magonjwa, tiba na uzuiaji. Tuliangazia matini
zinazohusiana na sehemu tulizotaja kama zinavyodhihirika katika hospitali ya Kisii Level 5.
Matatizo tunayorejelea ni ya kiisimu na yale yasiyokuwa ya kiisimu. Katika hospitali ya Kisii
Level 5 kuna kikundi kiitwacho ‘Quality Improvement Team’ ambacho hujihusisha na kutafsiri
matini hizi. Tafsiri hizi ni za kihuduma na ziko katika mabango, maagizo yaliyoandikwa,
maelezo, vijikaratasi vya maelezo na vijitabu.
Tafsiri za kimatibabu ni swala linalohitaji uangalifu mkubwa kwa kuwa huathiri afya ya
mwanadamu. Kwa sababu ya kuchanganyika kwa watu kutoka jamii mbalimbali, tafsiri husaidia
kupitisha ujumbe kutoka lugha moja hadi nyingine. Wadensjo (1998) anadai kuwa katika nchi
nyingine, tafsiri zinazohusiana na sheria, afya na elimu zimeendelezwa kama taaluma za kiusomi
(TY). Anaendelea kusema kuwa ni dhahiri kwamba wataalamu wa kimatibabu hawawezi kutoa
huduma za kuridhisha za kiafya ikiwa hawawezi kuwasiliana vyema na wateja wao(uk 88,
uk88). Hivyo basi tafsiri za kimatibabu ni jambo ambalo haliwezi kufanywa bila umakinifu
unaohitajika. Gambier (2001) anadai kuwa tafsiri si kitendo rahisi cha kupitisha ujumbe kutoka
lugha moja hadi nyingine ila ni kitendo changamano kinachohusu uakifishaji, njia za kueleza
wakati, tarehe na mahali (TY). Maelezo haya ya Gambier yanawiana vyema na tunachosisitiza
kuhusiana na tafsiri za kimatibabu. Vipengele alivyovitaja Gambier kama vile kuzingatia
uakifishaji na wakati ni swala muhimu katika tafsiri za kimatibabu. Ushauri wanaotoa
wahudumu wa kimatibabu huathiriwa na maelezo na wakati kwa mfano, tiba hasa kuhusu tembe
huwa na maelezo ya wakati. Mtafsiri apitishe ujumbe usiokuwa na utata wa maagizo na maelezo
katika karatasi za tembe. Badala ya kutaja kuwa tembe zitumike asubuhi, mchana na jioni, ni
vyema kutaja wakati mahususi kama saa moja jioni kwa kuwa jioni huanza saa kumi.
Citation
Moraa Lydia (2013). Matatizo Yanayodhihirika Katika Matini Tafsiri Za Kimatibabu: Utafiti Kielelezo Katika Hospitali Ya Kisii Level5Publisher
University of Nairobi