Fonolojia ya nomino-mkopo za kikamba kutoka Kiswahili
Abstract
Utafiti huu umechanganua taratibu za utohozi wa nomino za Kikamba kutoka Kiswahili
kwa madhumuni ya kuainisha kanuni zinazohusika. Uchanganuzi umeongozwa na
mtazamo wa Fonolojia ya vipande sauti huru ambao ni mojawapo ya mitazamo ya
Fonolojia Zalishi. Kulingana na mtazamo huu, fonolojia ni mfumo sauti wenye rusu nne:
rusu msingi, rusu fonimu, rusu silabi na rusu toni. Nadharia ya Mawimbi pia ilitumiwa
kueleza sababu zilizochangia ukopaji katika lugha ya Kikamba. Utafiti wetu umeainisha
nomino za Kikamba zilizokopwa kutoka Kiswahili, ukabainisha vigezo vya kifonolojia
vilivyotumika na kuchanganua taratibu na kanuni za kifonolojia zilizofuatwa katika
ukopaji huo. Vigezo vya fonolojia ya Kikamba ambavyo ni fonimu, silabi na sifa arudhi
vimebainishwa. Pia, sababu zilizochangia ukopaji katika lugha ya Kikamba zimeelezwa.
Data msingi ya utafiti ilikusanywa katika sehemu ya Kitui ya kati kupitia mbinu za
mahojiano na uchunguzi wa kushiriki. Katika uwasilishaji, maelezo yameambatana na
michoro na majedwali. Uchunguzi umedhihirisha kwamba katika kushughulikia maneno
mkopo, mbinu tatu huhusika nazo ni: uchopekaji, udondoshaji na ugeuzaji maumbo.
Utafiti wetu una nafasi ya kuchangia uwanja wa isimu lugha ya Kiafrika kwa jumla
tukizingatia kwamba utohozi unaweza kutumika katika kulinganisha mifano ya fonolojia.
Pamoja na haya, data ya matokeo ya uchunguzi wetu inaweza kuwasaidia wasomi wa
isimu za lugha za Kiafrika. Vile vile, matokeo ya utafiti huu yanachangia kukua kwa
lugha ya Kikamba kwani uchunguzi ulishughulikia mabadiliko yaliyofanyiwa maneno
yaliyokopwa na hii ni njia moja ambayo lugha hutumia kukuza msamiati wake
Citation
Shahada ya uzamili katika idara ya Kiswahili ya chuo kikuu cha NairobiPublisher
University of Nairobi