Matumizi Ya Lugha Katika Kanisa Katoliki: Uchanganuzi Wa Ubadilishaji Msimbo Katika Mahubiri
Abstract
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuangalia matumizi ya lugha katika Kanisa Katoliki kwa
kuchanganua ubadilishaji msimbo katika mahubiri. Utafiti ulitumia data iliyokusanywa kwa
kurekodiwa katika makanisa teule matatu kwa kutumia nadharia ya Umaanisho ya Grice (1975).
Tuliongozwa na haipothesia zifuatazo; kwanza, kuwa ubadilishaji msimbo katika diskosi ya
mahubiri unaathiri maana katika kiwango cha matumizi ya elementi za kiisimu. Pili, wahubiri
katika Kanisa Katoliki hubadilisha msimbo. Tatu ubadilishaji msimbo katika diskosi ya mahubiri
husababisha ukosefu wa urasmi na nne kiwango cha elimu, tabaka, tajriba, cheo na umri
husababisha mabadiliko ya jinsi lugha inavyotumika. Ilithibitika kuwa ubadilishaji msimbo
katika diskosi ya mahubiri unaathiri maana katika kiwango cha matumizi ya elementi za kiisimu,
na kwamba wahubiri katika Kanisa Katoliki hubadilisha msimbo kwa wingi katika mahubiri
ambapo ubadilishaji huu husababisha ukosefu wa urasmi. Aidha elimu, tabaka, tajriba, cheo na
umri husababisha mabadiliko ya jinsi lugha inavyotumika.
Tasnifu hii ina sura tano. Sura ya kwanza imeshughulikia kwa muhtasari kile kinachofanywa
katika utafiti huu kwa kutoa mwelekeo jinsi utafiti wenyewe utakavyofanyika. Sura ya pili
imeshughulikia ubadilishaji msimbo kwa kuzingatia mbinu na mikakati mbalimbali.
Imeshughulikia pia msingi wa ubadilishaji msimbo na aina za ubadilishaji msimbo. Majukumu
na athari za ubadilishaji msimbo pia zimezingatiwa. Baadaye ufungamano wa misingi ya
ubadilishaji msimbo na Kanisa Katoliki umeshughulikiwa. Sura ya tatu na ya nne zimehusika na
uchanganuzi wa data kwa kutumia vijenzi na msingi wa nadharia ya Umaanisho juu ya
ubadilishaji msimbo wakati wa mahubiri katika Kanisa Katoliki. Sura ya tano ni hitimisho na
muhtasari ambapo tumetoa maoni na mapendekezo.