dc.description.abstract | Tasnifu hii ni juu ya uchanganuzi kimaudhui na kimtindo wa mchezo wa‘Papa Shirandula’
unaoonyeshwa katika runinga ya ‘Citizen’. Mchezo huu umetungwa na Charles Bukeko na
ulipeperushwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2007 lakini haujafanyiwa uchanganuzi wa
aina yoyote kimaudhui na kimtindo. Mchezo huu unasimulia maisha ya Papa Shirandula
ambaye pia huitwa Wilberforce anayefanya kazi ya bawabu katika kampuni ya Anderson
Holdings Company Limited. Papa Shirandula ni mhusika matata anayeunda mbinu nyingi
ili kujikimu kimaisha na mara nyingi hutumia uwongo na hila ili afaidike si ajabu kwa
majirani zake na mkewe Wilbroda yeye ni “meneja mkurugenzi” ilhali kwa hadhira ni
bawabu.
Utafiti huu umefungua ukurasa wa uchambuzi wa mchezo huu kwa kushughulikia maudhui
na mtindo. Tumeshughulikia maudhui na vipengele vyake kama vile dhamira, falsafa,
maadili na ujumbe. Katika mtindo tumejadili vipengele vya ploti, muundo, mandhari,
wahusika na toni. Mwongozo wetu katika tasnifu hii ni nadharia ya umuundo ambayo
huangalia jinsi kipindi hiki kilivyosukika kimaudhui na kimtindo ili kutimiza malengo
yake. Pia, katika kazi hii tumeonyesha matokeo ya utafiti wetu na kisha kutoa
mapendekezo tuliyoona yanafaa.
Kazi hii imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza ni utangulizi unaoeleza mada ya
utafiti, madhumuni ya tasnifu, sababu za kuchagua mada hii, upeo na mipaka, msingi wa
nadharia, nadharia tete na njia tulizotumia kufanyia utafiti huu. Pia katika sura hii
tumerejelea kazi mbalimbali zilizofanywa kuhusu mada hii. | en_US |