Uchanganuzi Linganishi Wa Maswala Ya Vijana Na Jinsi Yanavyoshughulikiwa Na Waandishi Katika Diwani Ya Tunu Ya Ushairi
Abstract
Katika tasnifu hii tumeonyesha maswala ya vijana na jinsi yanavyoshughulikiwa na
waandishi katika diwani ya Tunu ya Ushairi ambayo ina mkusanyiko wa mashairi ya
waandishi wanne tofauti.Waandishi hawa ni pamoja na Andanenga, Nyanje, Kiponda na
Arege (2013). Utafiti huu umeonyesha kwamba vijana wana changamoto nyingi katika
jamii ambazo ni lazima hatua ya dharura ichukuliwe ili kuokoa kizazi kijacho.
Tumeshughulikia mashairi kumi na saba ambayo tulichagua kwa kutumia sampuli
lengwa. Katika utafiti huu, nadharia ya uhalisia imetumika kuonyesha ukweli wa mambo
katika jamii. Ukweli huu ni ule ambao unaweza kuonekana na kuthibitishwa pasi na
tashwishi yoyote ile. Nadharia hii ya uhalisia iliwezesha kuhakiki maswala ya vijana
katika jamii na jinsi waandishi wa diwani ya Tunu ya ushairi wanavyoshughulikia
maswala hayo. Maswala haya ni pamoja na elimu, ukosefu wa maadili, umaskini,
magonjwa, ukosefu wa malezi bora na ukosefu wa ajira. Baada ya kufanya utafiti wetu
kwa kina tuligundua kwamba ni kweli vijana katika jamii tofauti huwa na changamoto
sawa. Pia makisio yetu kuwa waandishi wote katika diwani ya Tunu ya ushairi wana
mwelekeo sawa kuhusu vijana ni kweli kwa sababu maswala wanayoyashughulikia ni
maswala ibuka katika jamii na yanawahusu vijana.
Publisher
University of Nairobi