dc.description.abstract | Utafiti huu umeshughulikia suala la upole kama linavyobainika katika matumizi ya lugha ya
wahusika wakuu katika tamthilia ya Mbaya Wetu. Mtafiti ametumia mtazamo wa Nadharia ya
Upole ya Brown na Levinson (1987) na kujikita katika kipengele cha mikakati ya upole. Data ya
uchunguzi huu ilitokana na uchambuzi wa kauli na matamshi ya wahusika wakuu katika
tamthilia ya Mbaya Wetu. Lengo la kwanza la utafiti lilikuwa kubainisha iwapo wahusika wakuu
katika tamthilia ya Mbaya Wetu wanaitumia mikakati ya upole katika kuokoa uso
wanapoingiliana. Matokeo yanadhihirisha kuwa, wahusika wakuu katika tamthilia ya Mbaya
Wetu wanaitumia mikakati ya upole wanapoingiliana kama njia ya kuyafanikisha mazungumzo
yao. Lengo la pili la uchunguzi huu lilikuwa kubainisha jinsi sifa za wahusika wakuu katika
tamthilia ya Mbaya Wetu zinavyobainika kupitia matumizi yao ya mikakati ya upole. Utafiti huu
unaonyesha kuwa, sifa mbalimbali za wahusika wakuu zikiwemo hasi na chanya zinabainika
kupitia matumzi yao ya mikakati ya upole.Vilevile, uchunguzi huu ulidhamiria kuzichunguza
hali zinazoyaathiri matumizi ya mikakati ya upole inayotumiwa na wahusika wakuu katika
tamthilia ya Mbaya Wetu. Matokeo yanaonyesha kuwa, matumizi ya mikakati ya upole na
wahusika wakuu katika tamthilia ya Mbaya Wetu yanaathiriwa na hali mbalimbali za kijamii
kama vile mamlaka na malengo yao. Kwa jumla, utafiti huu umebainisha kuwa, upole una nafasi
kubwa katika kuikamilisha kazi nzima ya tamthilia. Kupitia uchunguzi huu, imethibitika kuwa,
kufanikiwa kwa maingiliano ya wahusika katika tamthilia kunategemea kiwango chao cha matumizi ya mikakati ya upole. | en_US |