Uchanganuzi Wa Kimtindo Wa Zinguo La Mzuka Na Mbaya Wetu

View/ Open
Date
2015Author
Nyandiwa, Hudson
Type
ThesisLanguage
OtherMetadata
Show full item recordAbstract
Utafiti huu ulihusu uchanganuzi wa kimtindo katika Zinguo la Mzuka na Mbaya Wetu.
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuchunguza matumizi ya sitiari, chuku, tashbihi,
tashihisi, kejeli, tanakuzi na oksimora katika tamthilia zinazohusika. Tulichochewa na
ufahamu kwamba mtindo na dhana ya maudhui ni vitengo muhimu vya fasihi ambavyo
huandamana na kuegemeana ili kufanikisha dhamira ya mwandishi kwa wasomaji wa
kazi yake. Uchochezi huu ulikuwa na ukweli kwamba matumizi ya tamathali za usemi
huondoa uchapwa katika kazi za sanaa pamoja na kuwa matumizi ya tamathali za usemi
si ya kiajali ila hutumika kimakusudi. Matumizi ya tamathali hizi huwa ni kuwasilisha
ujumbe kimuktadha ili kuwezesha uelewa wa matini kwa kina. Utafiti uliongozwa na
nadharia ya elimumitindo inayohusu uchanganuzi wa mbinu zote za lugha ambazo
hutumika katika mawasiliano ambayo hujumuisha mawasiliano ya fasihi na mawasiliano
yasiyokuwa ya fasihi. Ni wazi kuwa tamathali za usemi za sitiari, chuku, tashbihi,
tashihisi, kejeli, tanakuzi na oksimora husheheni maana zinapotumika katika muktadha
na bila muktadha ni vigumu kuchanganua tamathali yoyote kisemantiki. Kwa hivyo
matini huzipa muktadha wa uchanganuzi. Baada ya kuzisoma tamthilia hizi tulitambua
kuwa tamathali za usemi tulizotaja hapo juu zilitumika katika tamthilia za Mbaya Wetu
na Zinguo la Mzuka. Tulizichanganua kwa kurejelea muktadha wa matumizi yazo
kwenye matini hizi. Iligundulika kuwa matumizi ya vipengele vya tamathali za usemi vya
sitiari, chuku, tashbihi, tashihisi, kejeli, tanakuzi na oksimora vimechangia katika kuibua,
kuendeleza na kuwasilisha maudhui katika tamthilia zinazohusika. Kwa hivyo
iligunduliwa kwamba msanii hutawala lugha kiufundi ili kuonyesha tofauti kati ya lugha
ya fasihi na lugha ya kawaida. Aidha, tamathali za usemi hutumiwa na msanii
kimakusudi. Kwa hivyo ujumbe ulioko kwenye tamathali hizi huwasilishwa kwa
kuzingatia muktadha na vilevile, ni vigumu kuchanganua usemi wenye ukiushi ambao
hutokea katika hali isiyokuwa na muktadha. Isitoshe, iligundiliwa kwamba ukiushi katika
tamathali za usemi huwezesha uelewa wa kina wa matini. Muktadha wa kiisimu
huchangia kutoa maana ambayo mwishowe huibua na kuwasilisha maudhui na kwa hivyo
kuifanya kazi ya sanaa kuwa na maudhui ya pekee kutokana na ukiushi kwenye usemi
huo na mwisho lugha huwa na uwili usioepukika, yaani uwakilishi wa maana ya kisanii
na maana ya kimawasiliano. Napendekeza na kutilia mkazo kwamba vipengele vya fani
kama vile muundo, wahusika na mandhari vichunguzwe katika tamthilia hizi mbili.
Vilevile ukiushi wa kisintaksia, kileksika na wa kisarufi waweza kuchunguzwa. Aidha,
nadharia tofauti na tuliyotumia yaweza kutumiwa.
Publisher
University of Nairobi